Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema uwepo wa taarifa sahihi za kijiolojia za miamba umebeba dhana ya utajiri na maisha bora kwa Watanzania na kwamba dhana ya Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini kwa kutengeneza matajiri wengi kupitia Sekta ya Madini sambamba na kuboresha maisha ya Watanzania.
Mavunde ameyasema hayo hii leo Novemba 10, 2023, jijini Dodoma, ili kutimiza malengo hayo, Serikali imekuja na mkakati wa kuiongezea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania – GST na utafiti wa kina wa miamba yote yenye madini iliyopo hapa nchini kwa lengo la kutengeneza kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia.
Amesema, “malengo yetu ni kufanya tafiti za kina kwa angalau asilimia 50 kufikia asilimia 2030, ukilinganisha na sasa ambako ni asilimia 16 pekee ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kwa kutumia teknolojia ya kisasa, unaweza kuona mchango mkubwa iliyonao sekta ya madini pamoja udogo wa sehemu iliyofanyiwa utafiti wa kina wa miamba, sasa tukifanya mara tatu ya hapo tutakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi sambamba Pato la Taifa kwa ujumla.”
Mavunde amesema, “tafiti hizi zitatuonesha sehemu maji yalipo, maji safi na salama ni muhimu kwa maisha ya watu wetu, lakini pia Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kujenga mabwawa 100 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua zisizotabirika pia madini ya jasi yanasaidia kuondoa tindikali kwenye ardhi kwa ajili ya kilimo, mpaka hapo unaweza kuona jinsi sekta ya madini inavyogusa maisha wa Watanzania kupitia kilimo na maji.”
Ameongeza kuwa, taarifa za tafiti hizo pia zitafungamanisha Sekta ya Afya kwa kuwa zitasaidia kujua miamba yenye gesi ya Hellium ambayo inatumika katika teknolojia ya upigaji picha za kina za anatomia (MRI), vipimo vinavyotumika hospitalini, na hivyo kuonesha jinsi sekta ya madini inavyoenda kugusa sekta ya afya.
Aidha, ameongeza kuwa uwepo wa taarifa hizo zitasaidia kuondoa migogoro baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwasababu chanzo cha migogoro hiyo ni wachimbaji wadogo kuamini madini yapo kwenye maeneo ya wachimbaji wakubwa kwa kuwa yamefanyiwa utafiti wa kina, hivyo migogoro hiyo itaisha baada ya kupata maeneo mengine yaliyofanyiwa tafiti .