.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN ameahidi kuwa serikali  itanunua mashine MBILI za kisasa za mionzi kwa ajili ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wanaoenda kupata matibabu katika Taasisi hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara fupi ya kutembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na Kumtembelea na kumpa pole Katibu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Saleh Ramadhani Feruzi ambaye anapatiwa matibabu kwenye Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mkakati uliopo wa serikali unalenga kuhakikisha kuwa hali ya utoaji wa huduma za afya na dawa kote nchini unaimarika maradufu ili wananchi waweze kupata huduma hizo kwenye maeneo yao kwa ubora unatakiwa.

Kuhusu uhaba wa wahudumu wa afya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN ameuahidi uongozi wa Taasisi hiyo kuwa serikali itahakikisha wahudumu hao wanapatikana katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Baadhi ya wagonjwa na wananchi wamepongeza utoaji wa tiba katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na wameomba serikali iendelee kuipatia taasisi hiyo vifaa vya kisasa vya kutolea tiba kama hatua ya kuboresha utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu ya saratani.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

29-Jul-16

TRL Yafanya Mabadiliko Safari Za Treni
Wallace Karia: Msiwe Wachoyo Wa Elimu