Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad ambaye pia ni mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwakilisha Ukawa, amekanusha taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amejiuzulu.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chadema jana jijini Dar es Salaam, Maalim Seif ambaye pia ni makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, alieleza kuwa taarifa hizo ni uzushi uliotengenezwa na gazeti ambalo linamilikiwa na mtu asiyewatakia mema kisiasa.

“Gazeti mwalijua la nani..! Hao ambao wanaotaka kutuchafua, kutukoroga. Mimi ndiye katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF). Na katiba yetu ya chama inasema waziwazi , kiongozi wa ngazi ya taifa au ngazi yoyote ile akitaka kujiuzulu anaandika barua kwa Katibu kwa mamlaka iliyomteua. Kwa kuwa sasa alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF, mimi ndio Katibu wa Mkutano Mkuu wa CUF lakini mpaka dakika hii sijapata barua yake ya kujiuzulu,” alisema Maalim Seif.

Aliongeza kuwa yeye na Profesa Lipumba wamekuwa na mawasiliano ya karibu na kwamba juzi majira ya saa nne usiku walikuwa pamoja na alimpa salamu zake ili azifikishe kwa wajumbe wa mkutano huo kwa kuwa yeye asingeweza kuhudhuria.

Katika hatua nyingine, Seif Sharif alikanusha tetesi zilizoenea hususan upande wa Zanzibar kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atavunja muungano.

Alisema msimamo wake kuhusu muungano ni kutumia muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na katiba ya wananchi iliyopelekwa bungeni na tume ya Jaji Joseph Warioba na sio kuuvunja muungano.

Mkutano Mkuu wa Chadema ulipitisha rasmi jina la mgombea wake wa urais, Edward Lowassa na Mgombea Mwenza, Juma Haji Duni aliyehamia katika chama hicho akitoa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa lengo la kukidhi matakwa ya kisheria kupata nafasi hiyo.

 

Benzema Aendelea Kushawishi Usajili Wake Arsenal
Sunday Oliseh Kuanza Kazi Kwa Vitendo Dhidi Ya Taifa Stars