Serikali imeipongeza Taasisi ya Wanyamapori Afrika kwa kuunga mkono jitihada za usimamizi wa wanyamapori na kupambana na biashara haramu ya ujangili nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja katika hafla ya kusherehekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya Wanyamapori Afrika.
“Tumekuwa tukishirikiana kwa pamoja katika kuendeleza uhifadhi na shughuli za usimamizi wa wanyamapori hasa katika kukomesha biashara haramu ya ujangili ikiwa ni pamoja na kuanzisha vitengo vya mbwa waliopatiwa mafunzo ya hali ya juu kutumika kukagua nyara kwenye viwanja vya ndege vya Kilimanjaro (KIA), Julius Nyerere (JNIA) na katika bustani na vituo vikuu vya usafiri,” Masanja amesisitiza.
Aidha, amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa viongozi wanaohusika na masuala ya uhifadhi barani Kiafrika na pia kushirikisha jamii katika masuala ya uhifadhi.
Katika hatua nyingine, Masanja ameipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa Maonesho ya Tuzo za Wanyamapori za Benjamin Mkapa za Afrika kwa mwaka 2021 yanayoonesha picha bora zaidi za asili zilizopigwa barani Afrika zinazosimulia hadithi ya uhifadhi ya Afrika kwa njia za ubunifu kwa kutumia kamera.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi Wastaafu na wadau wa Sekta ya Maliasili na Utalii.