Klabu ya Tabora United imekamilisha rasmi usajili wake kuelekea msimu Ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupata saini za wachezaji kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikiwemo TP Mazembe, Botswana, Burundi na Nigeria.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha Msaidizi wa timu hiyo Henry Mkama amesema wamefanya usajili wa nguvu ambao wanaamini utaleta chachu kubwa kwenye soka la Tanzania, huku wakiwa wana jumla ya wachezaji 26, wazawa 14 na wageni 12.
Kocha huyo amewataja baadhi ya wachezaji wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu Ujao kuwa ni John Noble kutoka Nigeria, Mutuale Nyongani kutoka Maniema ya DR Congo, Lumiere Banza Kalumba (TP Mazembe), Andy Bikoko Lobuka Sanga (Balende FC- DR Congo).
Wengine ni kiungo mshambuliaji Toauya Jean Didie kutoka Rajaa FC ya Burundi na Kelvin Kingu Pemba kutoka Mbabane Swallows ya Eswatini.
“Hali za wachezaji wetu wote ziko vizuri, wanaendelea na mazoezi chini ya kocha wetu Goran Kuponovic,” amesema Mkama.
Aidha, Afisa habari wa klabu hiyo Pendo Lema, amesema usajili walioufanya ni usajili mkubwa na wenye tija na utakwenda kuleta ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu msimu ujao.
Tabora United itacheza Ligi KuU Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu ujao utakaoanza Agosti 15, baada ya kupanda daraja msimu uliopita wakati ikijulikana kama Kitayosce FC.