Klabu ya Kitayosce ‘Tabora United’ inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imefungiwa kusajili katika dirisha hili la usajili mpaka itakapowalipa wachezaji wanaoidai.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’, uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Kimataifa la Soka ‘FIFA’ baada ya wachezaji husika kushinda kesi za madai dhidi ya klabu hiyo.
Inadaiwa kuwa wachezaj watatu wa kigeni walifungua kesi FIFA wakipinga kuvunjiwa mikataba kinyume cha taratibu na kutolipwa.
Klabu hiyo ilitakiwa iwe imewalipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hizo.
Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji Kimataifa, Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limeifungia klabu ya Kitayosce ‘Tabora United’ kufanya uhamisho wa ndani.
Katika hatua nyingine TFF imezikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.
TFF imeongeza kuwa iwapo klabu inataka kuvunja mkataba na mchezaji au kocha, inatakiwa kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu.