Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani – FAO, pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani, inafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Akizungumza kando ya warsha hiyo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Lukanga amesema tafiti hizo zitaibua taarifa za maeneo ambayo sehemu ya maziwa na Bahari ya Hindi nchini, ili kuweka taarifa zake sahihi kulingana na idadi ya watu ambao wamekuwa wakinufaika kupitia rasilimali zilizopo.
Amesema, kwa sasa idadi ya watu nchini imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni sitini ila bado taarifa zilizopo kwenye sekta ya uvuvi zinatolewa kulingana na idadi ya watu iliyokuwepo zamani ya zaidi ya milioni 40, ambayo imekuwa ikibainisha watu wanaojishughulisha moja kwa moja katika sekta ya uvuvi ni milioni 4.5.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania – TAFIRI, Dkt. Mary Kishe amesema taasisi hiyo ambayo mwaka huu inafikisha miaka 40 imekuwa ikikusanya na kutafiti masuala mbalimbali ya sekta ya uvuvi, lakini bado haijaangalia mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa na mtu mmoja mmoja.