Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kujikita kwenye tafiti zenye tija kwa wavuvi wadogo na kushauri vyema kwenye mamlaka za serikali juu ya njia mbalimbali zikiwemo za kiteknolojia ili sekta ya uvuvi iwe na tija zadi kwa mvuvi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja Jijini Dar es Salaam kujionea namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

Akiwa katika ofisi za TAFIRI zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Ulega amefafanua kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo ni lazima zijibu changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo, hivyo ni muhimu kufikiria mambo ya kufanywa ili kuondoa changamoto zilizopo ikiwemo ya zana za uvuvi kutokana na mazingira ya sasa.

Aidha, ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezeko la watu na mahitahi ya samaki, TAFIRI inapaswa kufikiria kwa kina zaidi kwa kufanya tafiti nyingi zaidi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI), ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania hususan wadau wa sekta ya uvuvi wananufaika kupitia tafiti zenye matokeo chanya kwao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei ameelezea changamoto kwa Naibu Ulega kuwa taaisisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hali inayosababisha kushindwa kufikia baadhi ya malengo waliyojiwekea katika tafiti kutokana na ukosefu wa vifaa vikiwemo vya maabara.

Hata hivyo Dkt. Kimirei amesema licha ya changamoto zilizopo TAFIRI imeendelea kuhakikisha inafanya tafiti ambazo ni muhimu kwa sekta ya uvuvi ili kuwa na taarifa sahihi juu ya sekta hiyo ili taifa liwe na dira ya kufahamu rasilimali za uvuvi zilizopo katika Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo hapa nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), (hawapo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na kuwataka wafanye tafiti zenye tija kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo juu ya zana za uvuvi na teknolojia ya kisasa ya kufahamu maeneo yenye samaki.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akitoa taarifa fupi kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega , mara baada ya kufika katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, ambapo ameelezea changamoto za kifedha zinavyowarudisha nyuma katika kufanya tafiti.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), mara baada ya Naibu Waziri Ulega kumaliza ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaaam.

KMC FC, MASITA SPORTS WEAR zasaini mkataba
Ulega ataka TAFICO kujiendesha kibiashara