Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo amesema chama hicho kinajivunia mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka sitini ya Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba tisa mwaka 1961.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Lumumba mkoani Dar es Salaam, Chongolo amesema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini ndani ya kipindi cha miaka sitini ya Uhuru ni kufikishwa kwa huduma za kijamii karibu na Wananchi.
Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na afya, elimu, maji na miundombinu, ambapo kwa sasa Watanzania wengi wa maeneo ya mijini na vijijini wanapata huduma hizo.
Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa amewashukuru Viongozi wakuu wote walioliongoza Taifa ndani ya kipindi chote cha miaka 60, kwa kuwa uongozi wao umezingatia misingi ya umoja, amani na mshikamano, misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.