Wizara ya Afya nchini Tanzania, imetoa tahadhari kuhusu ugonjwa wa Ebola ambao unasemekana kulipuka Nchi jirani ya Uganda.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel katika Taarifa yake kwa waandishi wa habari amesema Septemba 20, 2022 Wizara ilipata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.
Taarifa hiyo, imeeleza kuwa mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola amefariki wilayani Mubende nchini Uganda ambapo alisemekana kuwa na dalili za homa kali, degedege, kutapika matapishi yenye damu, kuharisha na kutokwa damu machoni.
Taarifa za uchunguzi zinaonesha ugonjwa huu umesababishwa na kirusi cha Ebola aina ya Sudan (Ebola-Sudan strain) na kwamba “Uwepo wa ugonjwa huu katika nchi jirani unaiweka nchi yetu katika hatari kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu kupitia mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari,” amesema Dkt. Mollel.
Wizara imeongeza kuwa, dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni na machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi.
Dkt. Mollel amewatahadharisha wananchi kuwa “Ugonjwa huu unaenea kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa mfano mate, damu, mkojo na machozi. Endapo utapata au kuona mtu mwenye dalili hizi, unashauriwa kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya mapema.”
“Nimewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuimarisha utoaji wa elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalam na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kinga muhimu katika maeneo yao. Vilevile, nimewaelekeza kuimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka yetu ikiwemo matumizi ya vipima joto (thermal scanners).” ameongeza Dkt. Mollel.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini na kuwashauri wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kugusa mwili au majimaji ya mwili wa mhisiwa au mgonjwa wa Ebola, na kuepuka safari zisizo za lazima kutembelea maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huu.