Taharuki imezuka jijini Harare nchini Zimbabwe baada ya mwanamke mmoja anayejiuza (kahaba) kukiri kuwa hupeleka kwa mganga kondomu alizotumia na kwamba madhara huwapata wateja wake ikiwa ni pamoja na vifo.
Akizungumza katika kipindi cha ibada, mbele ya mhubiri maarufu ajulikanaye kama CB Motondo wa kanisa la ‘Grace Faith Ministries’ kilichorushwa moja kwa moja kwenye kituo cha runinga, mwanamke huyo aliyejitambulisha kama Lindie alidai kuwa alichukua hatua hiyo kama sehemu ya masharti ya mganga wake ili apate bahati na mvuto.
Alikiri kuwa yeye ni kahaba ambaye alianza kufanya kazi hiyo katika mgodi wa Chiadzwa, lakini aliona hafanikiwi na akaamua kujaribu sehemu nyingine katika mitaa ya Harare.
Mhubiri CB Mutondo alimueleza kuwa hata huko alikoenda anaona mambo yanazidi kwenda kombo na kwamba amechukua uamuzi ambao unawagharimu maisha wateja wake.
“Ninaona wanaume saba ambao alitembea nao [ambao kondomu zao alizipeleka kwa mganga] wote wameshafariki,” alisema Mhubiri CB Mutondo.
Lindie alikiri kuwa alipofika kwa mganga alipewa masharti na mojawapo ni kuhakikisha anapeleka kondomu alizotumia.
Mhubiri CB Motondo alieleza kuwa katika ulimwengu wa kiroho ameona kuwa kondomu hizo zimekuwa zikiwasababishia mikosi wanaume waliohusika, na kwamba wengine huishia kupoteza maisha. Mwanamke huyo alikiri kuwa baadhi ya wanaume alioshiriki nao na aliowasilisha kondom alizotumia nao kwa mganga walishafariki.
Mhubiri huyo amekuwa gumzo hivi sasa nchini Zimbabwe, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Hivi karibuni alizua gumzo baada ya kutabiri kuwa kuna rais mwanamke atakayeiongoza Zimbabwe.
Mtandao wa Zimbabwe wa Bulawayo ulimtafuta msemaji wa mhubiri huyo ambaye alieleza kuwa Jumapili hii atakuwa na neno la kinabii kwa Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini ikiwa ni pamoja na neno maalum kwa wanawake wa Zimbabwe.