Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars leo Alhamis (Septemba 07) itakuwa na kazi moja tu ya kusaka angalau pointi moja ili kuweka rekodi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya tatu katika historia ya nchi itakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya Algeria, huku Serikali ikiitakia kila la kheri.
Stars itashuka kwenye Uwanja wa Mei 19 uliopo kwenye mji wa Annaba Kaskazini mwa nchi hiyo majira ya saa 4:00 kwa saa za Afrika Mashariki, ikijaribu kurudia ilichokifanya mwaka 1979 na 2018 ilipofuzu kucheza AFCON ambazo Fainali zake zilichezwa 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri.
Ofisa Habari wa Mawasiliano wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo amesema kikosi kimejiandaa vyema kwani kiliwasili salama jana Jumatano (Septemba 06) kutoka mjini Tabarka nchini Tunisia na kilifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya pambano hilo, huku kikiwa na wachezaji wote, isipokuwa nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta ambaye alitarajiwa kuwasili baadae tayari kwa pambano hilo.
“Kikosi kimeshajiandaa na kiko tayari kwa mchezo huo, nia ya wachezaji, Benchi la Ufundi, Serikali na TFF ni kuhakikisha tunacheza fainali za AFCON kwa mara nyingine tena,” amesema Ndimbo.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma amesema mchezo wa leo una umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa sababu Stars inahitaji pointi moja tu iweze kufuzu bila kuangalia matokeo ya mechi nyingine.
“Mchezo huu una umuhimu mkubwa sana ukilinganisha na mingine mingi ambayo tumecheza katika miezi kadhaa huko nyuma kwa sababu sasa tunahitaji pointi moja bila kuangalia matokeo ya mechi nyingine, lakini pengine tunaweza kupata bahati Niger wakatoa hata sare na Uganda tukawa tumefuzu moja kwa moja,” amesema.
Stars inayohitaji ushindi au sare ipo kwenye Kundi F, ambalo linahitaji timu moja kuungana na Algeria ambayo tayari imefuzu kucheza Fainali hizo.
Msimamo wa kundi hilo kabla ya michezo ya leo, Algeria anaongoza akiwa na pointi 15 akifuatiwa na Taifa Stars wenye pointi saba huku Uganda wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne huku Niger ikiburuza mkia.
Kutokana na msimamo huo, Stars hata ikipata sare itakuwa imefuzu moja kwa moja Fainali hizo zitakazochezwa Ivory Coast hata kama Uganda itafanikiwa kuifunga Niger.