Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo kinaanza safari ya kuelekea Benin, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundi F wa kuwania kufuzu Fainali za AFCON 2023 dhidi ya Niger.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Benin keshokutwa Jumamosi (Juni 04) majira ya jioni, huku Stars ikiwa na matumaini ya kupambana ugenini na kupata ushindi, ambao utakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Stars ilianza kambi mwanzoni mwa juma hili jijini Dar es salaam, huku wachezaji wote walioitwa kikosini na Kocha Kim Poulsen wakiitikia wito kwa haraka.
Niger itacheza nchini Benin, kufuatia Uwanja wao Seyni Kountché kukosa vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’, hivyo itachza michezo yote ya kuwania kufuzu, katika nchi jirani.
Baada ya mchezo wa Jumamosi, Stars itarejea nyumbani Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi F dhidi ya Algeria, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Juni 08.
Mwezi Septemba, Stars itaendelea na mchakato wa kusaka nafasi ya kucheza Fainali za AFCON 2023, kwa kucheza dhidi ya Uganda ugenini.