Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limetangaza ratiba maalum ya maandalizi kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyoanza kambi jana Jumapili (Mei 29) Jijini Dar es salaam.
Taifa Stars inakabiliwa na michezo miwili ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Niger, utakaopigwa Juni 04 nchini Benin kisha itakutana na Algeria jijini Dar es salaam Juni 08.
TFF imetangaza ratiba hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ikionyesha Taifa Stars itaondoka jijini Dar es salaam siku mbili kabla ya mchezo dhidi ya Niger (Juni 02).
Baada ya kucheza dhidi Niger Juni 04, Stars itaanza safari ya kurejea jijini Dar es salaam Juni 05, kuendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Algeria utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 08.
Ratiba hiyo inaonyesha baada ya mchezo dhidi ya Algeria, Kambi ya Stars itavunjwa na wachezaji kuruhusiwa kurudi kwenye vilabu vyao kwa ajili ya kuendelea na Ligi Kuu Tanzania Bara.