Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Jumatatu (Machi 15) itashuka dimbani kuvaana na timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaopigwa kwenye uwanja wa Nyayo, Nairobi nchini Kenya.
Michezo hiyo itatumika kama sehemu ya maandalizi kuelekea michezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) dhidi ya Equatorial Guinea na Libya itakayochezwa baadae mwezi huu.
Kocha Mkuu wa Tanzania, Kim Poulsen amesema: “Tumejiandaa vizuri kwa mchezo wa Leo wa kirafiki dhidi ya Kenya. Tumefanya mazoezi ya kupiga pasi, kupokea pasi pia na katika hali ya kawaida timu iko vizuri
“Tuko tayari kwa kucheza kandanda safi na kila mchezaji yuko tayari kwa mchezo kutoka na mazoezi yaliyofanyika,” alisema Poulsen
Naye kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
Tanzania itacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Harambee Stars huko Kenya. Baada ya mchezo wa leo, timu hizo zitarudiana siku tatu baadae katika uwanja wa Kasarani.