Sentahafu wa Young Africans, Kelvin Yondani si miongoni mwa wachezaji 18 walioondoka leo Septemba mosi, 2016 kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).

Taarifa ambazo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezipata ni kwamba Yondani ana matatizo ya kifamilia ambako hajayaweka sawa hadi timu hiyo inaondoka kwenda Nigeria na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa hajajaza nafasi hiyo.

Mkwasa amekerwa na kitendo hicho, lakini TFF itasubiri ripoti ya kocha huyo mara baada ya kurejea kutoka Nigeria.

Timu hiyo imeondoka na wachezaji 18 huku ikitarajiwa kuungana na na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta nchini Nigeria. Samatta – Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji anatokea jijini Brussels ambako makocha wake wamemwomba Mkwasa na Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba kumwangalia namna ya kumtumia kwa sababu ya uchovu wa mechi nzito zilizoipa matokeo mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya Uropa Ndogo.

Taifa Stars inakwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles utakaofanyika Septemba 3, 2016.

Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

Wachezaji waliosafiri:

Makipa: Said Kipao(JKT Ruvu) na Aishi Manula (Azam FC)

Mabeki: Vicent Andrew, Mwinyi Haji (Young Africans), Mohamed Hussein (Simba SC), Shomari Kapombe na David Mwantika (Azam FC)

 Viungo: Ibrahim Jeba – Mtibwa Sugar, Himid Mao(Azam FC), Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Muzamiru ( Simba SC), Juma Mahadhi (Young Africans) na Farid Mussa Tenerif ya Hispania.

Washambuliaji: Jamal Mnyate, John Bocco(Azam FC), Ibrahim Ajib (Simba SC) na Simon Msuva (Young Africans).

Viongozi waliosafiri na timu: Ahmed Mgoyi (Mkuu wa msafara), Charles Boniface Mkwasa (Kocha Mkuu), Hemedi Morocco (Kocha Msaidizi) Hussein Swedi (Mtunza Vifaa), Richard Yomba (Daktari wa timu)

Magufuli agusia mpango wa kubadili ‘fedha’ kuwakomoa waliozificha
Henrikh Mkhitaryan Yu Shakani Kuwakabili Man City