Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo imesafiri kuwafuata wapinzani wao Libya mchezo wao wa pili wa kufuzu michuano ya Afcon inayotarajiwa kufanyika nchini Cameroon 2021.
Sars itamenyana na Libya nchini Tunisia ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 2-1 dhidi ya Equatorial Guinea mchezo uliochezwa jana uwanja wa Taifa.
Kwenye msafara huo nyota Erasto Nyoni ambaye ni kiraka ameachwa nchini kwaajili ya matibabu ya goti.
Etienne Ndayiragije, Kocha Mkuu wa Stars amesema kuwa ameachwa Nyoni kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata jana kwenye mchezo dhidi ya Equatorial Guinea.
Stars imeanza vyema michuano ya Afcon kwa kuibuka kidedea mbele ya timu ya Equatorial Guinea kwa kupata ushindi huo ambapo mchezo uliochezwa uwanja wa Taifa.
Stars iliyo chini ya Ndayiragije ilianza kwa kasi kipindi cha kwanza haikuweza kutumia vema nafasi saba za kipindi cha kwanza na kuruhusu wapinzani wao Equatorial Guinea kuandika bao la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa Pedro Obiang liliwapeleka Stars mapumziko wakiwa nyuma.
Kipindi cha pili Stars ilianza kwa kulazimisha mashambulizi na iliwapeleka mpaka dakika ya 68 ambapo Simon Msuva aliandika bao la kwanza akimalizia pasi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kuweka mzani sawa.
Salum Abubakari alimaliza ile fujo isiyoumiza dakika 90 kwa kulipa mbao wa Obiang akiwa nje ya 18 kwa kuachia mshuti wake wenye uzito uliomshinda mlinda mlango wa Equatorial Guinea akimalizia pasi ya Ditram Nchimbi.