Mmiliki na Rais wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint Germain Nasser Al-Khelaifi ametajwa kuwa mpango wake ni kuona beki wa timu hiyo, Sergio Ramos anasalia kikosini hapo, ila kwa masharti.
Ramos ambaye ni beki mzoefu anatarajiwa kumaliza mkataba wake ndani ya Paris Saint- Germain mwishoni mwa msimu huu, huku wengi wakiendelea kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyoifanya akiwa na Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Real Madrid.
Mpaka sasa Ramos bado hajapewa dili lolote jipya ndani ya kikosi hicho licha ya kutakiwa na baadhi ya timu za Uarabuni na Marekani.
Lakini maamuzi ya kusalia kwa beki huyo kikosini hapo yatajulikana mwisho wa msimu pale Mkurugenzi wa Ufundi, Paris Saint-Germain, Luis Compas atakapofanya maamuzi juu ya hatma yake japo rais katoa mapendekezo yake.
Paris Saint-Germain kuelekea msimu ujao inasaka beki wa kati na Aymeric Laporte wa Manchester City akitajwa pamoja na beki wa kushoto Lucas Hernandez ndiyo wamekuwa wakijadiliwa huko Paris.
Ramos alisajiliwa kama mchezaji huru akitokea Real Madrid kwa mkataba wa miaka miwili, lakini msimu wake wa kwanza Paris alitumia kuuguza majeraha.