Tajiri wa Klabu ya Chelsea Todd Boehly ameripotiwa alilazimika kujifungia ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na wachezaji kwa muda wa saa nzima baada ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Brighton mwishoni mwa juma lililopita.

Bosi huyo raia wa Marekani alichukizwa na kichapo kingine katika mchezo wa Ligi Kuu England iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge juzi Jumamosi (April 15).

Sasa Brighton imeichapa Chelsea ndani na nje msimu huu na kuweka rekodi mbovu hata baada ya Graham Potter kufukuzwa kazi huku ikiendelea kujikita katika nafasi ya 11 kwenye msimamo.

Lakini licha ya Frank Lampard kurejea kama Meneja wa muda The Blues mambo yameendelea kuwa magumu kwa sababu amechezea kipigo cha tatu mfululizo tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo ya mpito.

Kwa mujibu wa ripoti baada mchezo dhidi ya Brighton, Tajiri huyo alikwenda kwenye vyumba vya kuvalia ili akawape makavu wachezaji wake kufuatia kipigo hicho.

Bosi huyo aliungana na mmiliki mwenzake Behdad Eghbali, na wakajifungia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji wa Chelsea kabla ya kuondoka uwanjani.

Tukio hilo lilikuja huku picha zake zikisambaa mtandaoni zikimuonyesha akibishana na mashabiki wa Chelsea baada ya mchezo huo kumalizika.

Mashabiki kadhaa wa Chelsea waliokuwepo karibu na bosi huyo walionekana wakibishana naye na kumnyooshea vidole baada ya kichapo.

Senyamule ahimiza amani, amuombea Rais Samia
Mawaziri sekta ya uvuvi, ukuzaji viumbe maji EAC wakutana