Takataka zilizorundikwa na kutengeneza rundo la mlima wa mita 15 limeanguka na kusababisha vifo vya watu 17 katika eneo la Helene, kilomita 10 kutoka jiji la Maputo nchini Msumbiji.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu wiki hii ambapo nyumba zilizokuwa katika maeneo hayo zilizikwa na uchafu huo majira ya saa tisa usiku.
Serikali imewahi kuwatahadharisha wakaazi wa eneo hilo ambao walijenga kinyume cha sheria na kuwataka waondoke lakini hawakuitikia wito huo. Uchafu huo uliorundikwa kwa miongo kadhaa umeporomoka wiki hii kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika jiji hilo.
Kiongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ka Mavota, Despedida Rita aliwaambia wandishi wa habari kuwa bado inaaminika kuna miili iliyofunikwa na uchafu.
“Miili 17 imepatikana. Inahofiwa miili zaidi inaweza kuwa imefukiwa na uchafu. Hivyo, tunaendelea kutafuta miili kwa kufukua uchafu,” alisema Rita.
Imeelezwa kuwa changamoto ya upatikanaji wa ardhi kwa wakaazi jijini humo imesababisha wakaazi wengi kuishi katika maeneo ambayo hayakubaliki kisheria.