Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans Salum Abdallah Mkemi ameingia matataji baada ya kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Wilaya ya Rufiji kwa Tuhuma za Rushwa.
Mkemi anahusishwa na utoaji wa Rushwa kuhusiana na Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani. Inadaiwa anajiandaa kugombea jimbo la Rufiji.
Mkemi anakuwa Mwanamichezo wa Pili kuingia kwenye mzozo na TAKUKURU kuhusiana na Rushwa ya Uchaguzi baada ya Katibu Mkuu wa zamani wa FAT (TFF), mwenyekiti wa zamani wa Simba SC na mbunge wa zamani wa jimbo la Tabora Mjini Ismael Aden Rage.
Rage alishikiliwa na TAKUKURU na kufanyiwa mahojiano na baadae aliachiwa baada ya kutoa utetezi ulioridhisha mbele ya viongozi wa taasisi hiyo mkoani Tabora.
Mkemi alikua mjumbe wa kamati ya utendaji ya young Africans wakati wa utawala wa mwenyekiti yusuph Manji, lakini alitangaz kujiuzulu kabla ya uongozi huo kumaliza muda wake.
Hata hivyo jopo la uongozi wa Yusuph Manji liliishia njiani baada ya wajumbe wote wa kamati ya utendaji kutangaza kujiuzulu, na kutoa nafasi kwa klabu ya Young Africans kufanya uchaguzi uliowaingiza madarakani viongozi wa sasa chini ya mwenyekiti Mshindo Mbette Msolla.