Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, Mkoani Shinyanga, Donasian Kessy ameomba ukaguzi maalum kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali – CAG, kwa ajili ya kuchunguza mkopo wa Shilingi 900 milioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kessy ameyasema hayo hii leo Mei 25, 2023 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya taarifa ya kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa Fedha 2022/2023 ya TAKUKURU.
Amesema walipofanya uchunguzi wa awali walibaini fedha hizo kuwekwa kwenye akaunti tofauti tofauti hivyo wameomba kibali maalum kwa CAG ili kuweza kukamilisha uchunguzi huo.
Mkopo huo, ulikopwa toka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upimaji wa viwanja 2000.