Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imejibu madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa inatumika kisiasa, baada ya kuwahoji baadhi ya wabunge wa chama hicho kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zilizokuwa zikikatwa kwenye mishahara ya wabunge pamoja na michango.
Taarifa iliyotolewa jana na Afisa Mahusiano wa taasisi hiyo, Doreen Kapwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Brigedia Jenerali, John Mbungo imeeleza kuwa Takukuru ni chombo kinachojitegemea na kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Imewataka wanachama wa Chadema kuendelea kutoa ushirikiano kuhusu tuhuma hizo kwa sababu wanatakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007.
“Takukuru inawashauri wanachama wa Chadema kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi unaendelea,” imeeleza taarifa hiyo.
Kapwani ameeleza kuwa wanachama wa Chadema ndio waliowasilisha malalamiko yao wakihoji matumizi ya fedha zilizokuwa zinakatwa kwenye mishahara ya wabunge wa viti maalum na wabunge wa majimbo.
“Hatua hii ni muendelezo wa uchunguzi unaofanywa na Takukuru Makao Makuu kuhusu malalamiko juu ya matumizi ya fedha za chadema, ambapo hatua ya sasa ni kuwahoji wabunge 69 wa chama hicho pamoja na wanachama wa zamani wa chama hicho,” imeongeza taarifa hiyo.
Takukuru walianza kuchukua hatua kuhusu tuhuma hizi baada ya waliokuwa wabunge wa chama hicho waliohamia vyama vingine kudai kuwa walikuwa wanakatwa mishahara yao tangu Juni 2016.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika malalamiko hayo ilidaiwa kuwa kila mbunge wa viti maalum wa Chadema alikuwa anakatwa Sh. 1,560,000 kwenye mshahara wake wa mwezi, na wabunge wa majimbo walikatwa Sh. 520,000 kwa kila mwezi kwenye mshahara wake.