Mchezaji na Kocha wa zamani wa Simba SC Talib Hilal amesema Young Africans wanapaswa kujipanga kikamilifu ili kufikia lengo la kuibuka na ushindi dhidi ya watani zao wa jadi, katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumamosi (Mei 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Talib ambaye aliipa ubingwa Simba SC mwaka 2007 kwa kuifunga Young Africans kwa changamoto ya Penati katika michuano ya Ligi ndogo, Uwanja wa Jamuhuri mkoani Morogoro amesema mchezo wa Jumamosi utakua na taswira ya ushindani, lakini upande mmoja una kazi kubwa ya kufanya ili kufanikisha matokeo yanageuka na kuwa tofauti.
Mdau huyo wa soka ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Oman ya soka la Ufukweni, amesema Simba SC wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo, kutokana na mazingira waliyoyapitia msimu huu.
“Ukiangalia performance ya Simba kwa mechi za Ligi mpaka Ligi ya Mabingwa Afrika, wako vizuri sana na wanafanya vizuri. Mwaka huu wana timu nzuri licha ya kuyumba katika mechi mbili za mwanzo za ligi lakini baada ya hapo wakatudi kwenye form yao mpaka sasa hivi wanaendelea vizuri.”
Ukiangalia mechi ya Simba na Young Africans siku zote haitabiriki tangu huko nyuma, nguvu inatumika zaidi lakini kwa sasa Simba ipo vizuri. Kimahesabu Simba wako vizuri kushinda mechi hiyo lakini kiuhalisia inategemea dakika 90.
“Young Africans wanapocheza na Simba si sawa na Young Africans inapocheza mechi dhidi ya timu nyingine. Jinsi Simba wanavyocheza sasa hivi na performance yao, nawapa nafasi kubwa ya kushinda.”
Simba SC inaongoza msimamowa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 61, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 57 huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 54.