Wapiganaji wa Taliban leo wametangaza kuanzisha mashambulizi mfululizo katika kiipindi cha kiangazi, wakisisitiza kuwa wataendelea kupambana hadi vikosi vyote vya kigeni viondoke nchini Afghanistan.
Tamko la Taliban ambalo limekazia oparesheni maalum ya ‘Al-Fath (Ushindi)”, limeeleza kuwa malengo ya oparesheni hiyo ni “kuondoa kabisa uwepo wa vikosi vya kigeni nchini humo, kuanzisha utawala wa Kiislam na kuwalinda waamini wenzetu wa nchi Takatifu ya Kiislam.”
Tamko hilo limeongeza kuwa, “ingawa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu imeshaachiwa huru na maadui, bado kuna vikosi vya kigeni vinavyoendeleza shughuli za kijeshi na siasa katika nchi yetu ya kiislam.”
Katika kipindi kilichopita cha baridi, Taliban walikuwa wakishambulia vikosi vya Nato pamoja na vile vya Serikali ya Afghanistan kila siku.
Marekani imekuwa ikifanya mazungumzo mara kadhaa na Taliban ili kumaliza vita ambayo imeduni kwa kipindi cha miaka 17. Hii ni vita ya muda mrefu zaidi kuwahi kupiganwa na Marekani ikishirikiana na Serikali ya nchi husika. Maandalizi mengine yanaendelea kwa ajili ya kuandaa mazungumzo kati ya viongozi wa Serikali ya Afghanistan na wale wa Taliban katika jiji la Doha nchini Qatari.
Marekani bado ina wanajeshi 14,000 nchini Afghanistan na Rais Donald Trump ameonesha kutoendelea kutekeleza ahadi ya mtangulizi wake ya kupunguza idadi hiyo kama sehemu ya kutafuta muafaka.