Kundi la Taliban limefanikiwa kushika jiji la sita muhimu katika eneo la Kaskazini mwa Afghanistan, hatua inayoipa wakati mgumu Serikali ya nchi hiyo katika kujihakikishia usalama wake.
Jana, Taliban waliteka jiji la Aybak in Samangan, likiwa jiji la sita muhimu ndani ya kipindi cha siku nne tu.
Taarifa zinaeleza kuwa wapiganaji hao wanaendelea kufanikiwa kwa kasi, hadi jana jioni walikuwa wamelizunguka jiji lingine la saba la Mazar-i-Sharif, ambalo ni muhimu sana na liko katika eneo la Kaskazini.
Taliban inalivizia zaidi jiji la Kabul ambalo ndilo makao makuu ya nchi hiyo, na wakifanikisha watakuwa wameing’oa Serikali ya Afghanistan iliyokuwa ikilindwa na Marekani.
Marekani imekuwa kimya kufuatia hatua zinazoendelea na Rais Joe Biden ameweka wazi kuwa oparesheni ya jeshi lake nchini Afghanistan imefika ukingoni.
Mwezi ulipita, Taliban ililikamata jiji la Kandahar ambalo ni jiji la pili kwa ukubwa. Majeshi ya Serikali yalizidiwa nguvu na hawakuelewa waelekee wapi baada ya kipigo walichopokea kutoka kwa wapiganaji wa Taliban.
Taliban iliwahi kuiongoza Serikali ya Afghanistan baada ya kuiondoa madarakani Serikali iliyokuwepo. Baadaye, ikaondolewa na Marekani wakati wa harakati za kumsaka Osama Bin Laden aliyekuwa ndani ya nchi hiyo.
Kundi hilo chini ya Mullah Omar lilikataa wito wa Marekani wa kuwakabidhi Osama Bin Laden, wakaambulia kipigo kikali na kuondolewa madarakani.
Wapiganaji wa Taliban walibaki kuwa lisilochoka kuitafuta fursa ya kurejea kuiongoza Serikali na kuiondoa Serikali iliyokuwepo ambayo ilikuwa mshirika wa Marekani.