Kundi la Taliban limeitaka Marekani kusikiliza wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres wa kuziachilia fedha za Afghanistan zilizoko Marekani, wakati ambapo mzozo wa kibinaadamu ukiongezeka.
Maafisa wa Marekani walizuia mali za Afghanistan zenye thamani ya mabilioni ya dola, baada ya kundi hilo lenye itikadi kali kuchukua madaraka mwezi Agosti baada ya kuondoka kwa majeshi ya kigeni.
Jana, Guterres aliitaka Marekani kuongoza katika kuzuia mzozo wa kiutu unaojitokeza Afghnistan kwa kuziachilia fedha hizo.
Msemaji wa serikali ya Taliban, Zabinullah Mujahid amesema Marekani inapaswa kuitikia vyema sauti ya kimataifa na kuziachia fedha hizo.
Marekani imechukua udhibiti wa takribani dola bilioni 9.5 ambazo ni mali ya Benki Kuu ya Afghanistan.
Hata hivyo Mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa yamekadiria kuwa zaidi ya nusu ya watu milioni 38 wa Afghanistan wanatarajiwa kukumbwa na njaa katika msimu huu wa baridi.