Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, Aretas Lyimo amesema wengi wa Vijana wamekuwa wakijiingiza katika matumizi na uuzaji wa Dawa za kulevya kutokana na tamaa ya kujipatia fedha na wengine bila kutambua na kujua madhara ya wanachokifanya.
Kamishna Jenerali Lyimo ameyasema hayo wakati akiongea na Dar24 Media jijini Dar es Salaam kuhusu zoezi la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya sheria zinazoongoza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, madhara na aina ya Dawa za kulevya.
Amesema, wamekuwa wakijiingiza katika matumizi na uuzaji wa Dawa za kulevya kutokana na tamaa ya kujipatia fedha na wengine bila kutambua na kujua madhara ya wanachokifanya kutokana na wale wanaowadanganya kuwa ni mizigo ya kawaida wanabeba.”
Hata hivyo, Lyimo ameongeza kuwa ni vyema kuwa na uhakiki wa mzigo unaopewa kubeba au kupeleka sehemu na itasaidia kuepukana na madhara au kushiriki uhalifu kwani wengi wa wanaokamatwa wamekuwa hawana uelewa wa kile wanachosafirisha kutokana na kurubuniwa na wasambazaji wa Dawa za kulevya.