Klabu ya Simba inapenda kutoa taarifa kwa wanachama,wapenzi wake na washabiki wa mchezo wa mpira wa miguu kote nchini kuwa tamasha la kila mwaka la klabu yetu linalojulikana kwa umaarufu wa Simba Day lipo pale pale na wala ‘halijapeperushwa’ kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini.

Ni upotoshaji mkubwa usiozingatia weledi na maadili ya taaluma kulikopitiliza kulikofanywa na chombo hicho ambao unaweza kuleta athari kubwa kwa tamasha letu ambalo ni sehemu ya sherehe muhimu ya kuadhimisha miaka themanini toka kuanzishwa kwa klabu yetu yenye historia ya kutukuka ndani na nje ya mipaka yetu kupita klabu yoyote nchini.

Katika ratiba ya tamasha letu hili kesho kutakuwa na shughuli ya usafi kwenye mtaa wa Msimbazi yalipo makao makuu ya klabu na shughuli hii itaanza saa mbili kamili asububi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mbunge wa jimbo la Ilala yalipo makazi ya klabu Mh Mussa Azzan Zungu.

Tunawaomba wana Simba wote mjumuike kwenye jambo hili muhimu ambalo pia ni maagizo ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.Mh John Pombe Magufuli.

Pia hiyo kesho Jumamosi ya tarehe 6-8-2016 itakuwa ni siku ya kupiga picha za msimu kwa wachezaji na benchi zima la ufundi la klabu ya Simba.

Jumapili ya tarehe 7 ni siku ya wachezaji na benchi la ufundi kuwa live mitandaoni kwa kuperuzi na wana Simba kuhusina na masuala mbali mbali.

Sambamba na mkutano na wanahabari kati ya makocha na manahodha wa klabu ya AFC Leopard ya Kenya na sisi wenyeji wao Simba SC.

Kilele cha sherehe zenyewe ni siku ya Jumatatu tarehe nane mwezi huu pale uwanja wa Taifa hapa jijini kutakapokuwa na mechi kabambe baina yetu na Leopards.

Mbali ya mechi hiyo ambayo itawatambulisha wachezaji wote wa msimu huu wa Simba pamoja na mchezaji Laudert Mavugo ambae tayari yupo kambini.

Pia kutakuwa na burudani mbali mbali za muziki na sanaa

Siku ya kilele viongozi mbali mbali watahudhuria huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda.

Sanjari na viongozi hao, viongozi wote wa Simba wakiongozwa na Rais wa klabu Evans Aveva watashiriki kiukamilifu shughuli zote za tamasha hili kubwa kupita lolote linalohusisha vilabu vya soka kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Niwajulishe tu viongozi wetu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida huku tukiwaachia vyombo vya uchunguzi vikiendelea na kazi zao.

Klabu haitaki kuingilia kwa namna yoyote ile uchunguzi wa Takukuru na inaamini itajiridhisha na nia ‘NJEMA’ ya kamati ya utendaji ya klabu ya Simba.

Mwisho ingawa sio kwa umuhimu nitumie fursa hii pia kuwashukuru watanzania wote kwa dua na sala zao kwangu binafsi kwa kupata maradhi ya macho ambayo kwa kiwango kikubwa sana yamenusurika kwa jitihada za madaktari wa Tanzania na nchini India.

Jitihada zao zilikubaliwa na Mwenyezi Mungu ambae bila shaka alizikubali dua na sala zenu

Asanteni sana watanzania wenzangu.

Imetolewa na

HAJI S.MANARA

MKUU WA HABARI

SIMBA SPORTS CLUB

SIMBA NGUVU MOJA

Hakuna Messi, Neymar Wala Suarez
Video: MOI yakanusha taarifa iliyotolewa na gazeti la Mwananchi