Baada ya Mahakama ya Usuluhishi masuala ya Michezo dunaini (CAS) kuiamuru klabu ya Young Africans kumlipa Amisi Tambwe dola 20,000 sawa na Shilingi Milioni 46.4 za Tanzania, mshambuliaji huyo kutoka nchini Burundi amesema ikiwa hatalipwa fedha hizo, viongozi wa klabu hiyo kongwe watajuana na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa kuwa yeye hausiki kwenye kutoa hukumu.
Young Africans imetakiwa kumlipa Tambwe fedha hizo, ambazo alikuwa anaidai klabu hiyo kama ada ya usajili na mshahara wa miezi mitatu.
Tambwe amethibitisha kupokea taarifa kutoka kwa mwanasheria wake kwa kusema kuwa, kesi yake dhidi ya Young Africans ameshinda, hivyo kinachotakiwa ni kulipwa fedha zake anazodai.
“Mwanasheria wangu ameniambia kwamba tumeshinda kesi hivyo kinachotakiwa ni Young Africans kulipa hizo fedha kama hawatalipa ni wao watajuana na FIFA mimi sijui itakuaje.
“Tulichokifanya tumewapa akaunti namba Young Africans kisha tunasubiri kuona fedha zinaingizwa. Tena zinapaswa kuingizwa zote kwa kuwa ingekuwa kidogo kidogo ni wakati ule tungekubaliana ila kwa sasa hilo halipo.” Amesema Tambwe.
Mshambuliaji huyo aliachwa na Young Africans msimu wa 2018/19 kwa kile kilichoelezwa kuwa amechukua ubora wake. Tambwe aliondoka Young Africans akiwa na madeni yake hayo ambayo klabu hiyo haikumlipa kwa wakati kiasi cha kuwashitaki CAS na chombo hicho kutoa hukumu alipwe ndani ya siku 45 kuanzia Desemba 1, 2020.