Ofisi ya Rais – TAMISEMI imesema imeona taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikimuhusisha Mwanafunzi Sifika Daniel Ruben, wa Shule ya Sekondari ya Mkombozi iliyoko Wilaya ya Same, Kilimanjaro na kupangwa kidato cha tano Sekondari ya Namwai kuwa nafasi yake amepewa Mwanafunzi mwingine, hivyo yeye kukosa haki ya kuendelea na masomo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -TAMISEMI, Nteghenjwa Hosseah imeeleza kuwa TAMISEMI imefuatilia taarifa hizo kutoka Mkombozi Sekondari alikosoma Mwanafunzi huyo, hadi Shule ya Sekondari Namwai alikopangiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

“Anayelalamika mitandoni anaitwa Sifaeli Tawel Elirehema na alisoma Shule moja na Sifika Daniel Ruben, hata hivyo Binti huyo namba yake ya mtihani ilikuwa ni S.850/135 na alipata Div IV: 34 (Zero), alisoma masomo ya Sanaa ilhali Sifika Daniel Ruben namba yake ya mtihani ni S.850/136 na alisoma masomo ya Sayansi akipata Division 1:10,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imezidi kufafanua kuwa, Binti anayelalamika mitandaoni alifikishwa Shuleni na Walezi wake akiwa hana viambatanisho vyovyote na alipohojiwa ilibainika aliwadanganya Walezi wake jina na matokeo yake na Walezi hao waliomlea kama Msaidizi wa Nyumbani pasi na kufahamu ukweli wa taarifa walizopewa na Binti huyo.

“Hakuna aliyenyang’anywa haki yake ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na taarifa zilizotolewa na Binti huyo ni za uongo na zipuuzwe na Mwanafunzi Sifika Daniel Ruben anaendelea na masomo yake anayeonekana pichani ndiye Mwanafunzi Sifika,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha maelezo hayo yanazidi kufafanua kuwa Mwanafunzi huyo ndiye jina, namba na picha yake vimetumika kudanganya umma na yeye ndio ambaye yuko Shuleni aliyepata Division one “Wazazi/Walezi na wanaharakati msisambaze taarifa ambazo hamjajiridhisha na usahihi wake ili kuepuka kuzua taharuki.

JKT, NCAA wasaini makubaliano ujenzi Nyumba za Wananchi
Serikali yaanza kuchukua hatua upandaji bei za Vyakula