Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege ameridhishwa na matumizi ya fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Kinondoni zilizotumika katika utekelezaji wa miradi ya maedeleo iliyokamilika kwa wakati na viwango.
Amesema kuwa Manispaa hiyo ni mfano wakuigwa kwa kuwa imeonesha nidhamu nzuri katika matumizi ya fedha zinazotokana na vyanzo vya mapato ya ndani na kwamba miradi ambayo imetekelezwa kupitia fedha hizo inaendana na thamani halisia.
“Kimsingi leo nimemaliza ziara yangu katika Halmashauri hii, na kikubwa nilikuwa nimelenga zaidi kuona fedha zinazokusanywa na Halmashauri na namna ambavyo zinatumika katika miradi ambayo inaonekana na kimsingi naomba niwapongeze sana Kinondoni, mnazitendea haki fedha zenu mnazokusanya” amesema Kandege.
Kadhalika ameridhishwa na kiwango cha barabara zinazojengwa katika Halmashauri hiyo kupitia mradi wa DMDP na kusema kuwa kukamilika kwake kutaleta mafanikio makubwa kwa wananchi hususani watumiaji wa barabara ya Shekilango na kwamba itaondoa msongamano wa daladala na kuwawezesha wananchi kuondokana na adha ya foleni.
Amefafanua kuwa Mafanikio haya yanayoonekana leo Kinondoni ni kutokana na uongozi imara wa Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na usimamizi mzuri wa Mkurugenze Aron Kagurumjuli ulioleta tija kwa Wananchi.
Katika hatua nyingine ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kujenga kituo cha Afya katika Kata ya Kigogo na kusema kuwa walifanya mamuzi ya busara na yakujali wananchi kwakuwa eneo hilo halikuwa na Hospitali na kwamba litawasaidia wakazi hao kupata huduma bora ya afya.
Katika ziara hiyo Kandege ametembelea Barabara ya shekilango inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa shilingi Bilioni 14. 8, mfereji wa Kilongawima uliyopo Jimbo la Kawe kwa shilingi Bilioni 3.1 pamoja na upanuzi wa Zahanati ya Bunju mradi unajongekwa cha shilingi Milioni 600.