Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA, imeendelea kukabiliana na migogoro ya muingiliano wa maeneo ya Hifadhi na Wananchi ikiwemo kuhakikisha inalinda mipaka yake isiwe na muingiliano wa shughuli za Kilimo, Ufugaji na makazi unaofanywa na baadhi ya Wananchi wa maeneo jirani.
Hayo yamebainishwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wa Jeshi la Uhifadhi – TANAPA, Dkt. Noelia Myonga wakati akizungumza na Dar24 Medi a hii leo Jijini Dodoma na kusema hatua hiyo inatokana na baadhi ya Wananchi wasio waaminifu kuvamia maeneo ya hifadhi na kuanzisha shughuli za Kibinadamu.
Amesema, “Suala la muingiliano wa maeneo na Wananchi ni la miaka na kuna baadhi ya Wananchi wengine ni waelewa hufuata maelekezo ya Serikali, na baadhi yao wagumu kuelewa badala ya kuhama wao wanajisogeza katika mipaka ya hifadhi.”
Dkt. Myonga ameongeza kuwa, “sasa hivi tunaunda na kamati ili kutumia utaratibu watakao uelewa na kukubali kuhama kwa haraka na Serikali tayari imewekeza fedha katika kuhakikisha zinawekwa alama zinazoonekana zitakazomsaidia Mwananchi kuona mpaka kwa urahisi, ili kuondoa muingiliano kati ya Hifadhi na jamii.