Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa siku 14 kwa wateja wote wanaodaiwa kulipa deni la ankara za umeme endapo hawatafanya hivyo basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kukatiwa huduma ya umeme.
Hayo yamesemwa na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Tito Mwinuka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
“Shirika la umeme linashindwa kutekeleza majukumu yake mbalimbali kwa wakati ikiwemo uendeshaji wa shirika, matengenezo ya miundombinu pamoja na utekelezaji wa miradi, hayo yote yanasababishwa na malimbikizo ya madeni kwa wadaiwa sugu hivyo tunatoa siku 14, wasipoweza kulipa tutawakatia huduma ya umeme”. amesema Dkt Mwinuka.
Aidha, Tanesco imewataja wadaiwa sugu  ikihusisha Wizara na Taasisi za serikali zikiwa zinadaiwa zaidi ya bilioni 52.5, makampuni binafsi pamoja na wateja wadogo wanaodaiwa zaidi ya bilioni 94.9
Dkt. Mwinuka amesema shirika hilo linatarajia kuanza oparesheni maalumu ya kukusanya madeni hayo na matarajio yao ni kulipwa kwa malikimbizo yote ili yasaidie kujiendesha kiushandani na kwa ufanisi mkubwa zaidi na kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme nchini.
Hata hivyo, hatua hiyo imekuja ikiwa ni takriban siku 4 tangu Rais Magufuli kuagiza TANESCO kufuatilia madeni yote ikiwemo deni ambalo TANESCO inaidai ZECO, na kuitaka kuwakatia umeme wote watakaoshindwa kulipa kwa wakati

Taifa stars yapanda nafasi moja viwango vya FIFA
Lissu: Hatutakubali uchaguzi wa TLS usitishwe