Hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa siku 14 kwa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na taasisi za Serikali kuhakikisha wanalipa madeni yao ya umeme la sivyo watakatiwa umeme, vitaipa wakati mgumu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa Shirika hilo linadai wateja hao jumla ya Sh.275 bilioni.
“Tunadai kiasi kikubwa sana cha fedha kutoka kwa wateja wakubwa na wadogo wadogo, mpaka Zeco, hivyo tunatoa notisi ya siku 14 walipe deni lao kwani baada ya hapo tutasitisha huduma pamoja na kuchukua hatua nyingine za kisheria,” amesema Dkt. Mwinuka.
Aidha, Katika kiasi hicho, Zeco inadaiwa Sh. 127 bilioni ambacho ni sawa na asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka 2016/17 ambayo ni Sh. 841.5 bilioni.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wa Zanzibar, Salama Aboud Talib amesema kuwa hajapokea barua kutoka Tanesco hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.
Kuhusu wadaiwa wengine, Dkt. Mwinuka amesema hadi kufikia Januari, Shirika hilo lilikuwa linadai Wizara na taasisi za Serikali kiasi cha Sh52 bilioni huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa jumla ya Sh. 94 bilioni.
Hata hivyo, amesema kuwa malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya Shirika kwa wakati ikiwamo uendeshaji, matengenezo ya miundombinu pamoja na miradi mbalimbali.