Shirika la umeme nchini (TANESCO) Kanda ya Kati limetakiwa kuanzisha kitengo cha huduma ya haraka ili kuondoa vikwazo kwa wawekezaji na wenye viwanda wanaokuwa na uhitaji wa umeme wa uhakika.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge katika mkutano baina ya Tanesco, wawekezaji na wenye viwanda kutoka Mikoa ya Kanda ya Kati wenye lengo la kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Amesema pamoja na uwepo wa sera bado wanapaswa kuwa wabunifu kitu ambacho kitawezesha wawekezaji kupata kwa haraka huduma za umeme katika uzalishaji wao kimkoa na taifa zima kwa ujumla.
“Tunaelekea katika uchumi wa kati wa viwanda sasa ifike wakati muwe mnaenda mbali zaidi kwa kubuni mambo yenye manufaa kwa Taifa ili tupate uzalishaji wa kutosha unaotokana na shughuli za kimaendeleo kwa kuwapa kipaumbele wadau hasa wawekezaji,” amesema Dkt Mahenge.
Aidha, Dkt. Mahenge amesema ili wawekezaji wazidi kusambaa mkoani hapa ni lazima shirika hilo liboreshe huduma za umeme katika maeneo ya Wilaya za Bahi, Chemba, Kongwa na Mpwapwa sambamba na mji mdogo wa Kibaigwa na eneo la ranchi ya Taifa ya Narco.
”Mkifanya hivyo katika maeneo hayo ambayo yamekuwa yanaleta shida ya umeme mtakuwa mmesaidia kutatua changamoto za kila mara ambazo ni kikwazo katika shughuli za kimaendeleo kwa wakazi wa maeneo hayo na kwa wawekezaji” amefafanua Dkt. Mahenge.
Hata hivyo katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa amelipongeza shirika hilo la umeme Tanesco mkoa wa Dodoma kutokana na maboresho mbalimbali ya upatikanaji wa huduma za nishati kwa uhakika katika maeneo mbalimbali.
Awali meneja wa Tanesco kanda ya kati Mhandisi Atanas Nangali amesema wamelazimika kuitisha kikao hicho ili kuangalia namna wanavyoweza kuboresha mahusiano na huduma ikiwemo kufahamu changamoto zinazowakabili wateja katika ulipaji wa madeni.
“Historia ya Shirika letu inaonyesha wenye viwanda na wawekezaji wote wakubwa wamekuwa wakichangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la Shirika hivyo kikao hiki ni muhimu kuangalia namna bora ya kuboresha mahusiano kati yetu na wateja,” amefafanua Mhandisi Nangali.
Amesema katika kuboresha miundombinu Tanesco kanda ya kati inayohudumia mikoa ya Morogoro, Singida na Dodoma imeanza kufanya utanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Dodoma kutoka uwezo wa sasa Megawati 48 hadi kufikia megawati 400.
“Miradi mingine ni kituo kipya cha umeme kilichopo Ifakara mkoani Morogoro ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 16 na kituo cha Singida kitakachoongezewa uwezo kutoka megawatts 32 hadi 400,” amefafanua Nangali.