Uwekezaji wa Kituo cha Sayansi cha Stem Park kilichopo Mkoa wa Tanga katika mradi wa ufugaji Kuku na Majongoo Bahari, ulio chini ya usimamizi wa Project Inspire kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga na Wadau wa Maendeleo, utasaidia kuzalisha Wanasayansi mahiri katika Taifa.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua Miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amefurahishwa na uwekezaji huo wa Miradi 17 ukiwemo wa ujenzi wa Bustani ya kisasa ya mapumziko Jijini Tanga maarufu kama Forodhani, Kituo cha Sayansi Stem na ugaji huo wa Kuku na Majongoo Bahari.
Amesema, “uwekezaji huu mkubwa wa Kituo cha Sayansi Mkoani kwetu utatusaidia kupata wataalamu wengi hapo mbeleni, na kiukweli nimefurahishwa sana na kitu kikubwa kama hiki kuwepo hapa Mkoani Tanga.”
Aidha, Kindamba ameongeza kuwa Serikali imeweka Mazingira wezeshi ya Elimu kwa kuhakikisha kila Mtoto anaipata bila vikwazo, na kuwataka Wazazi kuhakikisha wanawapa haki hiyo Watoto wao.