Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeelekezwa kushirikiana na Balozi za Tanzania katika kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji hapa nchini.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab wakati alipotembelea Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Balozi Fatma ameongeza kuwa ili bidhaa za Tanzania ziendelee kuuzwa katika masoko ya kimataifa ulimwenguni, TanTrade inatakiwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Balozi za Tanzania katika kuhakikisha kuwa inatoa taarifa sahihi za bidhaa.
“Ushirikiano baina ya TanTrade na Balozi zetu uendelee kuimarishwa ili kuwawezesha wafanyabiashara kupata taarifa sahihi na kwa wakati, lakini pia ushirikiano huu utasaidia kutangaza fursa za biashara zilizopo nchini Tanzania katika Mataifa ya Kigeni,” amesema Balozi Fatma.
Balozi Fatma pia ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya maonesho ya Sabasaba kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi walioshiriki katika maonesho hayo ili kujua ni kwa namna gani wataweza kunufaika na fursa za kuuza bidhaa zetu kwenye nchi za kimataifa