Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika ya Kusini zimekubaliana kuimarisha na kukuza maendeleo ya sekta ya uchukuzi na usafiri wa anga baina ya nchi hizo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga Jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu majadiliano ya awali yaliyofanyika kati ya nchi hizo mbili juu ya mikataba mbalimbali inayotegemewa kusainiwa mapema hii leo.
Amesema kuwa katika majadiliano hayo wamejadili mikataba iliyowahi kusainiwa kwa kupima utekelezaji wake pamoja na kujadili mikataba mipya iliyojikita katika sekta mbalimbali za maendeleo zikiwemo za uchukuzi, nishati, elimu pamoja na mawasiliano.
“Katika sekta ya uchukuzi tumekubaliana kuboresha barabara, usafiri wa anga pamoja na reli hasa ya TAZARA, sisi tumenunua ndege na tunaendelea kununua zingine zitakazosafiri hadi Afrika ya Kusini hivyo nchi hiyo imekubali kuendelea kuwafundisha marubani wa Tanzania kuendesha na kukarabati ndege hizo,”alisema Balozi Mahiga.
Hata hivyo, ameongeza kuwa mikataba hiyo inayotarajiwa kusainiwa imelenga maeneo ambayo yatapewa kipaumbele katika ushirikiano huo yakiwemo ya uchumi, biashara na uwekezaji pia mikataba hiyo imewekewa utaratibu wa ufatiliaji na utekelezaji wake.