Serikali ya Tanzania na Algeria, zimesisitiza umuhimu wa kukuza Diplomasia ya uchumi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano – JPC, ngazi ya Wataalam unaoendelea jijini Algiers, Algeria.
Mkutano huo, utafuatiwa na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika Agosti 31, 2023 ambapo kwa pamoja ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika Agosti 1, 2023.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano ngazi Wataalam umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na kwa upande wa Algeria umeongozwa na Mkurugenzi Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Balozi Selma Haddadi Malika.
Akifungua mkutano huo, Balozi Shelukindo ameeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Algeria kuwa ni wa kihistoria na uliojengwa katika misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ahmed Ben Bella.
Amesema, Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa, pia inaendelea kujenga na ujenzi miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.
Naye Mwenyekiti Mwenza, Balozi Selma Malika katika hotuba yake amesema mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara, mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa mataifa yetu’’ alisema Balozi Selma Malika.
Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou ulilosababishwa na kuongezeka kwa joto kali.
Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara, viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia, mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.