Serikali za Tanzania na Cuba, zimekubaliana kushirikiana na kuimarisha misingi ya kisiasa, ujengaji wa uwezo kwa wanasiasa vijana, sekta za elimu, afya, utalii, biashara na uwekezaji.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, alipokutana na Balozi wa Cuba nchini, Yordenis Despaigne Vera, katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Amesema, “Tanzania imekuwa ikishirikiana na Cuba kwa muda mrefu na ushirikiano baina ya mataifa haya umekuwa imara tangu ulipooasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo Hayati Fidel Castro na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”

Balozi Mbarouk ameongeza kuwa kwa sasa Cuba imeonesha dhamira ya kushirikiana Tanzania katika kuimarisha misingi ya siasa, kuwajengea uwezo wanasiasa vijana pamoja na sekta nyingine kama vile elimu, afya, na utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji

Kwa upande wake Balozi wa Cuba nchini, Yordenis Despaigne Vera amesema kwamba Cuba inajivunia kuwa na uhusiano imara na Tanzania kwa takribani miaka 60 huku akisema Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha misingi ya kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Wakati umefika sasa kwa serikali zetu mbili (Cuba na Tanzania) kuimarisha ushirikiano wake kisiasa na kuhakikisha kuwa mataifa yetu yanakuwa na misingi imara ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi pia kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema Balozi Vera.

Kocha mpya Ivory Coast
Balozi Kairuki aaga akiwakaribisha Wachimbaji wa Madini