Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, amesema Umoja wa Afrika umeitengea Tanzania dozi milioni 17 za chanjo ya UVIKO- 19 kupitia mpango wa Umoja huo wa kuzisaidia Nchi wanachama kupata chanjo kwa ajili ya Wananchi wake.
Ameyasema hayo Addis Ababa Nchini Ethiopia alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Nchini Ethiopia (Diaspora) waliotaka kufahamu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na UVIKO -19 ikiwa ni pamoja na suala la chanjo.
Aidha Balozi Mulamula amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika Mashirika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa kusaidia upatikanaji dozi nyingine za chanjo ya UVIKO 19, ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata chanjo hiyo kutokana na mwamko wa Watanzania kuongezeka mara baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine Balozi Liberata Mulamula pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ethiopia Sahle – Work Zewde Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo Tanzania na Ethiopia zimekubalina kuendelea kutumia ndege za shirika la Ethiopia kutangaza vivutio na kusafirisha Watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja Tanzania.
Kwa upande wake Rais wa Ethiopia Sahle – Work Zewde amesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Nchi hiyo hususani katika kutatua changamoto zinazozuia maendeleo miongoni mwa Mataifa hayo.