Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) zimetia saini msaada wa mikataba ya miradi sita yenye gharama ya shulingi bilioni 307.9 itakayofadhiliwa kupitia mpango wa ushirikiano wa 11 chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya.
Hayo yamebainishwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James wakati wa hafla ya utiaji saini msaada huo Jijini Dodoma.
“Fedha hizi zinazotolewa na Umoja wa Ulaya zimekuwa chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ua uchumi,uboreshaji wa sera mbalimbali, miudombinu ya barabara,viwanja vya ndege, nishati, kilimo na mazingira,” aliongeza James.
James ameeleza kuwa misaada inayotolewa na Umoja wa Ulaya chini ya mpango wa 11 imeelekezwa kutatua mahitaji na changamoto zilizoainishwa katika mipango ya maendeleo ya kitaifa hususani Mpango wa Pili wa Maendeleo 2016/17-2020/2021 na MKUZA II.
Aidha, msaada huo umelenga kuendeleza miradi ya sekta ya Nishati, mradi wa matumizi endelevu ya nishati ya kupikia, mradi wa kusaidia mnyororo wa thamani katika ufugaji nyuki, kuboresha huduma ya afya ya mimea ili kuongeza usalama wa chakula, kuboresha mazingira ya biashara, na ushirikiano wa kitaalamu.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Balozi Mafredo Fanti amesema, “Utiaji saini wa mikataba hii utachochea ukuaji jumuishi, maendeleo katika Sekta binafsi na ajira, muingiliano wa uchumi na biashara, mabadiliko ya hali ya hewa.”
Tanzania na Umoja wa Ulaya ni washirika wa muda mrefu ambapo mpaka sasa Umoja huo umeshatoa misaada ya kifedha na mikopo ya masharti nafuu tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya kwanza ya ushirikiano kati ya umoja huo na nchi za Afrika Caribbean na Pacific (ACP) mnamo mwaka 1975 ambapo hadi sasa Tanzania imepokea shilingi trilioni 6.6 kama misaada na bilioni 748.2 kama mikopo ya masharti nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).