Tanzania ni nchi ya kumi duniani kwa uzalishaji wa nazi ikiongozwa nan chi ya Indonesia huku ikiwa ya kwanza Barani Afrika kwa kuzalisha wastani wa tani 530,000 kwa mwaka ikifuatiwa na Ghana ambayo huzalisha wastani wa tani 366,183 kwa mwaka.
Naibu waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amebainisha hayo jana na kusema kuwa mafuta mwali yatokanayo na nazi yanaendelea kupata umaarufu kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa ndani na nje ya nchi.
Amesema katika kuimarisha zao hilo la nazi nchini, msimu wa mwaka 2018/19 wakulima wapatao 74 katika mikoa ya Lindi na Mtwara wamefundishwa namna ya kukamua mafuta ya mwali.
Kikundi cha wanachama 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo kimepewa mashine yenye uwezo wa kukamua mafuta lita 500 kwa mwaka ambapo litamoja inauzwa hadi Tsh. 40,000/=.
Aidha amebainisha kuwa katika kuimarisha kilimo cha minazi nchini Serikali imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo kidogo cha utafiti chambezi wilayani Bagamoyo.
“Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa zao la nazi kuendelea kupanda mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na zenye tija kubwa” amesema Bashe.