Tanzania inategemea kuadhimisha siku ya Mazingira Afrika, Machi 3, 2017 ambapo siku hiyo imetengwa kukumbuka umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof.Faustine Kamuzora wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo Jijini Dar es Salaam juu ya maadhimisho hayo ambapo kitaifa yanategemewa kufanyika wiki ya kwanza ya mwezi wa sita.
Ameongeza kuwa Azimio la kuadhimisha Siku hiyo lilipitishwa na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri wa Mazingira wa nchi za Afrika (AMCEN) kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini mwaka 2002.
“Siku hii iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na kuenea kwa hali ya jangwa katika bara letu. Aidha siku hii ilikuwa inaadhimishwa nchini Ethiopia kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika,” amesema Prof. Kamuzora.
Aidha Prof.Kamuzora amewataka watanzania kushiriki katika maadhimisho hayo katika kukabiliana na uhalibifu wa mazingira unaosabishwa na matumizi yasiyoendelevu ya bioanuai na rasilimali zake.
Hata hivyo, Kamuzora amewakumbusha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kutumia fursa hiyo kuzihuisha kamati za Mazingira ili ziweze kusimamia shughuli za utunzaji mazingira katika maeneo yao ya Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Sekta zote pamoja na Taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya Kiserikali na Wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha wanahamasishwa kushiriki katika shughuli za hifadhi na usafi wa Mazingira.