Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa amesema Tanzania itaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO).
Ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Nchi Wanachama wa WIPO ulioanza tarehe 4 Oktoba na utahitimishwa tarehe 8 Oktoba, 2021 katika Mji wa Geneva, Uswisi
Katika hotuba yake, Bw. Nyaisa amebainisha miradi ya Miliki Bunifu ambayo nchi ya Tanzania imenufaika ikiwemo kujengea uwezo makundi mbalimbali ili kuweza kutumia Miliki Bunifu kwa maendeleo ya nchi .
“Mpaka sasa BRELA imeweka mfumo wa kushughulikia maombi ya hataza na alama za biashara (IPAS), mapitio ya sheria za Miliki Bunifu pamoja na vitabu na ufundishaji wa sehemu ya Shahada ya Uzamili ya Miliki Bunifu inayotolewa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam,” ameeleza.
Ameongeza kuwa, hivi karibuni WIPO na Mahakama ya Tanzania wamesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kwa nia ya kuimarisha mfumo wa mahakama na huduma za Miliki Bunifu na ulinzi nchini Tanzania.
Utekelezaji wa makubaliano hayo utasaidia kushughulikia changamoto za kisheria zinazohusiana na uamuzi wa Miliki Bunifu unaokabili mfumo wa Mahakama nchini Tanzania.
Mkutano huo utapitia na kujadili shughuli mbalimbali na kupitisha bajeti ya WIPO ikiwa Tanzania imekuwa mwanachama wa tangu mwaka 1983.