Tanzania imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Jumuiya ya nchi zilizo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association – IORA), katika kutekeleza mikakati ya uchumi wa bluu ambao unalenga kuimarisha sekta ya uvuvi, hususan uvuvi wa bahari kuu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki William Ole Nasha amesema hayo aliposhiriki Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi zilizopo katika jumuiya ya IORA uliofanyika Disemba 17, 2020 kwa njia ya mtandao.
Amesema Tanzania itaboresha Sekta ya Uvuvi kwa kuimarisha kilimo cha mwani, utalii wa meli (cruise tourism), michezo ya baharini, utafutaji wa rasilimali za mafuta na gesi kwenye eneo la bahari, ujenzi wa bandari maalum za uvuvi, mafuta na gesi na masuala mengine muhimu ya kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi.
Nasha ameeleza kuwa serikali ya Tanzania imejipanga kutumia rasilimali zilizopo katika bahari ya Hindi na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuwavutia na kuimarisha Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi.
Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo ya IORA umejadili masuala ya maendeleo katika eneo la Bahari ya Hindi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango kazi wa Jumuiya ya IORA wa mwaka 2017 – 2021.
Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa 22 wa Kamati ya Makatibu Wakuu/ Maafisa waandamizi wa Jumuiya ya IORA uliofanyika tarehe 15 – 17 Desemba, 2020.