Waziri mkuu, Kasim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia nchi ya Burundi ili ifanikiwe katika adhma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake .
Ameyasema hayo wakati wa mazishi ya Pierre Nkurunziza na kubainisha Tanzania na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao huo.
“Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa ametimiza kiu yake ya kutaka Burundi iwe mwanachama wa SADC jambo ambalo halikuwezekana naamini Mheshimiwa Rais utalisimamia suala hilo hadi litimie”amesema Waziri mkuuMajaliwa.
Rais wa Burundi, Ndayishimiye amesema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.