Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na fedha za Mfuko wa Kukuza Uwekezaji barani Afrika kutoka Serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi, 2023 kwa ajili ya mitaji (start-ups), zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwemo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya Keizai Doyukai (Japan Association of Corporate Executives), Mutsuo Iwai wakati akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo nchini Japan.
Amesema, “Ifikapo Desemba mwaka huu, tutazindua kampuni ya kusimamia mfuko huu wa uwekezaji wenye manufaa barani Afrika na utekelezaji utaanza Machi, 2023. Tunataraji ifikapo Machi, 2024 tutakuwa tumetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kwa kampuni za vijana wanaochipukia ili kuwajengea ubia, kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana ujuzi.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa hoteli za nyota tano na kuanzisha michezo ya majini kwenye fukwe za bahari Zanzibar na Bara. na kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye kilimo cha mashamba makubwa na ujenzi wa viwanda.
Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis, nchini Tunisia.
Mikutano hiyo ya Waziri Mkuu, ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda.