Serikali ya Tanzania itakuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wakuu wa nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Jumamosi Februari 27, 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 24, 2021 jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Mkutano huo wa Marais unatanguliwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaoanza kesho kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, mkutano huo utafanya uteuzi wa viongozi mbalimbali huku Mwenyekiti wa sasa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame atakabidhi kijiti kwa Mwenyekiti mpya atakayetangazwa Jumamosi.
Kabudi amesema Mkutano wa Wakuu wa nchi utahusisha uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa EAC, majaji wa mahakama ya haki ya EAC ngazi ya Mwanzo na Rufaa ikiwa ni pamoja na kumtangaza Rais na Makamu wa Rais katika ngazi hiyo.
Katika mkutano huo pia kutakuwa na uchaguzi wa Jaji Kiongozi ngazi ya kwanza ya mahakama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye takribani wakazi Milioni 170 inahusisha nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Sudan Kusini.